Kijana ni nani?

Unknown | 3:28:00 PM | 0 Maoni


Kijana ni mtu wa kike au wa kiume
mwenye umri kati ya miaka 15 na 45.
Biblia inasema nini juu ya kijana?
Biblia imenena mambo mengi juu ya
kijana, na baadhi ya hayo ni kuwa
fahari ya kijana ipo katika nguvu
zake (Mithali 20:29). Kijana ana
nguvu nyingi, neno la Mungu linakaa
ndani yake na kisha amemshinda
shetani(1Yohana 2:14b).

Yohana anawaandikia vijana akisema
wana nguvu nyingi, pili neno la
Mungu linakaa ndani yao na kisha
wamemshinda shetani. Nguvu
yaweza kuwa ya kiroho au ya kimwili,
maana zote ni za muhimu na mara
nyingine hutegemeana katika
utendaji.

Nguvu moja ikikosekana hujitokeza
upungufu unaoweza kupelekea
uharibifu kama vile mtu kurudi
nyuma kwa sababu ya majaribu.
Nguvu ya kimwili ya mtu wa Mungu
ikitumika kwa mujibu wa uongozi wa
Roho Mtakatifu, yaweza kupelekea
mtu kuwa na nguvu ya kiroho iletayo
ushindi juu ya hila na mitego ya
yule mwovu.Hapa ina maana kuwa,
kwa mtu wa Mungu ukiwa na nguvu
ya kimwili na unaongozwa na Roho
wa Mungu utamtumikia Mungu
pasipo ulegevu, tofauti na mzee
ambaye anaweza kuhitaji kufanya
jambo lakini nguvu ya kwenda
kufanya hana, hilo nalo Mhubiri
aliliona na kumhamasisha kijana
kutumika akiwa bado anazo nguvu.
Mhubiri12:1 ”Mkumbuke Muumba
wako siku za ujana wako kabla
hazijaja siku zilizo mbaya…“ Yohana
anawaandikia vijana akionyesha sifa
za aina ya vijana aliokuwa
akiwalenga. Anatazamia kwamba
kijana akiitumia nguvu hiyo kama
ilivyokusudiwa na Mungu, na
kulisoma neno, kuomba kwa bidii
zake zote, matokeo yake atakuwa na
hazina tele ya neno ndani mwake, na
kisha atamshinda shetani, maana
anazo nguvu za kiroho na za
kimwili. Kijana wa aina hii hana hofu
maana hata shetani akija kwa sura
gani au akitumia mazingira gani,
haogopi maana silaha alizo nazo
(Neno) ni tishio kwa adui. Mungu
anawatafuta vijana kama hao
wabebao silaha hiyo ya Bwana ,
nyakati zote, kila mahali na kwa
bidii. ”..Nimewaandikia ninyi
vijana, kwa sababu mna nguvu, na
neno la Mungu linakaa ndani
yenu, nanyi mmemshinda yule
mwovu “(I Yohana 2:14b).

Biblia inasema kijana akilitii Neno la
Mungu na kulifuata litasafisha njia
yake. Litamkamilisha kwa kiwango
anachotaka Mungu, kwa makusudi ya
Mungu na kwa utukufu wa Mungu.
Kwahiyo ili kijana aweze kuishi
maisha matakatifu, yenye ushindi
tele na yanayomtukuza Mungu
yampasa kuisafisha njia yake kwa
kutii, akilifuata neno la Mungu.
Zab.119.9 ” Jinsi gani kijana
aisafishe njia yake? Kwa kutii,
akilifuata neno lako.“

Kijana, kufanikiwa kuisafisha njia
yako kutategemeana na wewe
mwenyewe utakavyotumia nguvu
zako. Yakupasa kuelekeza nguvu zako
katika maombi, kujisomea Neno la
Mungu, hii ni pamoja na kulitafakari
na kulitendea kazi. Kwa kufanya
hivyo utapata nafasi nzuri ya
kumsikiliza Mungu na kujua ni nini
mpango na makusudi yake kwako.
Kijana hupaswi kulala usingizi tangu
jioni hadi asubuhi na tangu January
hadi Desemba, huo ni msiba wa
kutosha kwa kijana maana Biblia
inasema mtu wa aina hiyo atapata
umaskini wa kumtosha. Si vema
kijana kuzagaa, ukikutwa na adui
ukiwa umezagaa atakutumikisha
katika matakwa yake. Ni muhimu
sana kijana kuwa na mikakati na
kuiombea ili kupata uongozi wa Roho
Mtakatifu. Mungu anajali sana kijana
kuwa na mkakati. Mfano mzuri ni
namna alivyomwandaa Yoshua
kushika nafasi ya Musa. Awali ya
yote alimhakikishia uwepo wake
pamoja na kijana huyo, na
akamwahidi kutomwacha wala
kumpungukia kabisa: ”Hapatakuwa
mtu yeyote atakayeweza kusimama
mbele yako siku zote za maisha
yako…sitakupungukia wala
sitakuacha.“ (Yoshua 1. 5).

Hapa Mungu anamhakikishia Yoshua
kuwa, hata kutokee tatizo kubwa
kiasi gani , hata vitisho viwe vikubwa
namna gani, hata ainuke nani,
asingeweza kuzuia wala kukwamisha
kusudi la Mungu katika huduma
aliyokuwa anakabidhiwa na Mungu,
ya kuwafikisha Waisraeli nchi ya
Kanaani. Hali kadhalika wewe kijana,
yumkini bado unawategemea wazazi
au ndugu, lakini kwakuwa umeokoka
labda wamekutenga, hawataki
kukupa huduma, hata masomoni
unatishiwa kufukuzwa kwasababu
huna karo; yumkini umeoa au
umeolewa na huyo mume au mkeo
anakutesa kwa ajili ya wokovu; kazini
unanyanyaswa na mkubwa wako wa
kazi au wafanyakazi wenzio,
halikadhalika kwenye biashara zako
wanakutesa kwa njia mbalimbali.

Katika hali yoyote ile, jambo la
muhimu uwe na uhakika kwamba
Mungu yupo pamoja na wewe na
kwamba hatakuacha wala
hatakupungukia. Hivyo usikate
tamaa, azimia kutomwacha Mungu
kabisa , simama katika haki na ahadi
za Mungu, utaona ushindi mkubwa.
Baada ya Mungu kutoa uhakika juu
ya uwepo wake kwa kijana huyo
Yoshua, alimpa mikakati ya namna
atakavyoweza kufikia lengo ambalo
lilikuwa kuwafikisha Waisraeli katika
nchi ya ahadi, Kanaani. Mikakati hiyo
ni kama ifuatavyo:
1. Uwe hodari tu na ushujaa
mwingi….

Mungu hapendezwi na uvivu, alitaka
Yoshua awe hodari tu na ushujaa
mwingi na siyo mtu wa kujihurumia
hurumia bali awe mwepesi wa
kwenda anakotakiwa, kutekeleza
majukumu ambayo Mungu angempa
inavyotakiwa, kwa wakati unaotakiwa,
na pasipo hofu. Huo ndiyo ushujaa.
2. ...uangalie kutenda sawasawa na
sheria yote aliyokuamuru Musa
mtumishi wangu; usiiache, kwenda
mkono wa kuume au wa kushoto.
(Yosh. 1.7).

Mungu anamwambia Yoshua,
aangalie kutenda sawasawa na
sheria yote aliyokuwa ameamriwa na
Musa mtumishi wake Mungu. Swala
kuu hapa ni utii wa neno la Mungu.
Kwamba kijana hatarajiwi kuwa
msikilizaji tu wa Neno la Mungu na
kuendelea na maisha ya kidunia.
Kijana anahitajika kuwa msikiaji na
mtendaji/mtekelezaji wa maagizo ya
Mungu ndani ya Neno.

Mungu anasisitiza katika mstari wa
nane kuhusu kutafakari Neno.
Mungu alimtaka Yoshua, kuhakikisha
siku zote za maisha yake anafanya
Neno la Mungu kuwa sehemu ya
maisha yake. Alimtaka akiwaza awaze
(atafakari) Neno mchana na usiku,
maongezi yake yawe na msingi katika
Neno. Kuhusu kutendea kazi Neno,
Mungu alimwambia Yoshua aangalie
kutenda sawasawa na maneno yote
yaliyoandikwa humo (ndani ya
torati/Neno.

”Kitabu hiki cha torati kisiondoke
kinywani mwako, bali yatafakari
maneno yake mchana na usiku
upate kuangalia kutenda sawasawa
na maneno yote yaliyoandikwa
humo…."(Yoshua 1:8).

Kwa maana hiyo, iwe usiku iwe
mchana kijana saa zote unatakiwa
kutafakari neno la Mungu siyo
kuwaza shida, taabu na masumbufu
ya dunia hii. Kulitafakari Neno huja
baada ya kulisoma, Daudi alisema:
” Moyoni mwangu nimeliweka neno
lako, nisije nikakutenda
dhambi“ (Zab. 119.11).

Alilisoma na kisha akalihifadhi
moyoni. Neno hilo katika hazina ya
moyoni, likawa mshauri, mwongozo
na faraja wakati wa majaribu,
mapito au mateso. Na kwa kulitamka
likafanyika fimbo ya kumwangamiza
adui, na kufungua milango ya baraka
iliyofungwa na adui na pia
likatumika hata kubadilisha
mazingira kama Ezekia alivyotamka
uhai kwa mifupa, ikainuka ikiwa hai
na kuwa kikundi kikubwa cha watu.
Ili uwe na maisha yenye mwelekeo
wa ki-Mungu na ya mfano, epuka
kabisa kuwaza mambo mapotofu,
epuka mazungumzo mafu yasiyo na
uhai wa ki-Mungu maana
yatakuharibu wewe pamoja na
wakusikilizao, pia matendo yoyote
yaliyo kinyume na Neno la Mungu
epukana nayo. Mungu alijua kuwa
kijana huyu Yoshua asiposisitiziwa
na Mungu mwenyewe, asipoishi kwa
Neno ambalo ndiyo lishe bora ya
roho yake, angeharibikiwa, na hapo
kusudi la Mungu la ukombozi wa
wana wa Israel lingeyumba. Hali
kadhalika wewe usipoishi kwa kulitii
Neno na kufanya kama
linavyokuagiza, adui atayumbisha
mpango wa Mungu katika maisha
yako, matokeo yake ni
kuchanganyikiwa, kukata tamaa na
hata kufa kabisa kiroho. Lakini
ukisimama pasipo kujali mazingira
yanayokuzunguuka, Mungu anao
mpango mzuri sana na maisha yako
na ndiyo maana amekuokoa
(amekuita). Yumkini wewe ndiye wa
kwanza kumpa Yesu maisha yako
katika familia au ukoo wako. Mungu
anategemea kukutumia wewe
kulifikisha kundi hilo nchi ya ahadi
kama alivyomtumia Yoshua. Zoezi
hilo litafanikiwa iwapo utakuwa
hodari tu na mwenye ushujaa
mwingi, na kutenda sawasawa na
Neno kama linavyoletwa kwako na
Roho Mtakatifu mwenyewe kupitia
njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na
ujumbe huu unaousoma sasa.

Kipengele: ,

KUHUSU NEEMA MBISE MINISTRY:
Ni Mchungaji na mwimbaji wa nyimbo za injili hapa Tanzania!

0 Maoni