Kumfundisha Mtoto Habari za Mungu
Watoto wanajifunza sana kutokana na jinsi watu waliowazunguka
wanavyoishi/kuenenda. Vile vile wanajifunza kwa kuangalia picha na
michoro ya aina mbalimbali. Njia hizi ndizo zinafaa kutumika wakati
unamfundisha mtoto wa kuanzia mwaka mmoja habari za Mungu maana ndio
anaweza kukuelewa zaidi. Ni vyema ukaanza na umri huu mdogo kuliko
kusubiri akue zaidi ndio uanze kumfundisha habari za Mungu.
1. Omba na mtoto wako wakati wote, iwe chakula,
asubuhi ukiwa unaondoka/ameamka, wakati wa kwenda kulala au hata wakati
mnapotoka pamoja kwenda popote. Kwa kufanya hivi mara kwa mara taratibu
naye ataanza kuona kuwa maombi ni kitu cha muhimu na kadiri anavyokuwa
haitakuwa ngumu kumfundisha kuhusu umuhimu wa maombi. Nimeona jambo hili
kwa mtoto wetu Kenneth, kwa sababu ya mazoea ya kuomba pamoja amejenga
tabia hiyo na hata kama sipo akipewa chakula lazima kwanza afunge macho
na amumunye maneno kisha anasema ame ndipo anakula, vile vile anapoenda
kulala mchana, kwanza anamwambia dada ‘ aomba’ maana kuwa anaomba
kwanza ndipo alale. Biblia inasema mlee mtoto katika njia impasayo naye
hataiacha hata atakapokuwa mzee Mithali 22:6.
2. Msimulie hadithi za biblia kwa njia ya
kufurahisha huku ukiwa unamsomea biblia. Mwanzoni itakuwa ngumu
kukuelewa lakini kadiri unavyoendelea na kurudia rudia mara kwa mara
itakaa ndani yake na itamjengea tabia ya kusoma biblia ili ajue zaidi
zile habari unazomsimulia pale atakapokuwa anajua kusoma. Mnunulie
biblia ya watoto yenye hadithi fupi fupi za biblia na picha. Waweza pia
tafuta Video CD au DVD za hadithi za biblia kwa watoto na kuangalia
pamoja naye huku ukimsimulia, kwanza itakupa musa mzuri wa kukaa na
kufurahi na mtoto wako na huku ukimfundisha habari za Mungu aliye hai.
3. Imba naye nyimbo za kumsifu Mungu hasa zile
zinazopendwa na watoto. Mtoto tangia akiwa tumboni anapenda sana kusikia
mtu akimuimbia hasa kama ni mzazi wake, sio lazima utenge muda wa
kuanza kuimba na mtoto bali pale unapokuwa unamuogesha, unafua na yeye
anacheza nk tumia muda huo pia kumuimbia nyimbo za Mungu huku
ukimfundisha na yeye.
Mtafutie CD za picha na sauti za watoto
wanaomuimbia Mungu na mueleze kuwa wanaimba kwa furaha sababu
wanamuimbia Mungu. Hii itampa hamasa ya kumuimbia Mungu kama watoto
wenzie anaowaona na kuwasikia. Mwambie wanamwimbia Mungu sababu ni
mwema, anatupenda, ametuumba, anatupa chakula, ametupa wazazi nk. ili
aone uhalisia wa upendo wa Mungu.
4. Mfundishe kuonyesha shukrani pale mtu anapompatia
kitu au kumtendea jambo jema. Hata kama hajui kuongea mwambie tu sema
asante, mshukuru kwa sababu fulani, hii itamfundisha kuwa ukitendewa
jambo ni lazima kuonyesha shukrani. Mfundishe kumshukuru Mungu kwa
kuamka salama, kupata wazazi wa kumletea maziwa, kununuliwa toy mpya,
kumuona bibi n.k. Moyo wa shurani utamsaidia kumjua Mungu zaidi na kwa
hali hii atakuwa anatafuta mema ya kumshukuru Mungu kila siku.
5. Ishi maisha ya upendo, ukarimu na furaha wakati wote
ili mtoto aone uhalisia wa Mungu katika maisha yako. Nenda naye
kanisani na uwe unamwambia kwa nini huwa unaenda kanisani, kumshukuru
Mungu, kumuomba Mungu, nk. Usisahau kumpa sadaka naye awe anatoa huku
ukimweleza ni njia ya kumshukuru Mungu kwa vingi alivyotupatia.
Kumbuka kila mara kumkumbusha upendo wa Mungu, wema wa Mungu, ukuu wa
Mungu. Muonyeshe vitu mbalimbali na kumwambia kuwa Mungu
ameviumba(ameviweka) mfano ndege, wadudu, miti, maua, wanyama n.k. Ni
vyema mtoto akafahamu habari kamili za Mungu kabla hajaanza shule, hii
itakuwa ulinzi wake katika dunia hii ilivyojaa uharibifu.
Mungu atusaidie sana tunapowalea watoto wetu katika kweli ya Mungu. Amen.
Kipengele: Habari mpya, Mafundisho, Ujumbe wa leo
0 Maoni