Napenda kuimba kama ANN ANNIE

Unknown | 10:41:00 AM | 0 Maoni



Kama tulivyosema tangu mwanzo mwa mwaka huu kuwa utakuwa ni mwaka wa mabadiliko makubwa katika Injili hasa kwa waimbaji wapya.IK ilipata bahati ya kufanya mahojiano na mwimbaji wa nyimbo za injili hapa Tanzania NEEMA MBISE
 anayetamba na albamu yake ya "SINA CHA KUKUPA",ambaye aliweza kutueleza mambo mengi sana kuhusu yeye na muziki wa injili kwa ujumla. Hapa chini ni mahojiano kati ya IK na NEEMA MBISE:

IK:Hallow!

NEEMA MBISE:Habari yako mtumishi

IK:Salama tu za kwako? Nimekutafuta muda mrefu hupatikani!

NEEMA MBISE:Nilikuwa darasani na simu nilikuwa nimezima..

IK:Ok,twende moja kwa moja kwenye mada yetu.. Wasomaji wangependa kufahamu historia yako kwa ufupi tu..

NEEMA MBISE:Mimi tangu nimeanza muziki nina miaka mitatu,lakini kabla ya hapo nilikuwa naimba kwaya kanisani na shuleni,sunday school nilikuwa naimba pia.Hadi nilipopata wazazi wa kiroho ndipo nilipoweza kwenda studio kurekodi.Albamu yangu nimefanya na dada ANN ANNIEambayo inakwenda kwa jina la "SINA CHA KUKUPA"

IK:Nini kilichokuvutia sana hadi ukaamua kuingia katika uimbaji wa nyimbo za injili?

NEEMA MBISE:Nilikuwa napenda tu kuimba lakini nilikuwa sijajua kama nitakuja kuingia kwenye ulimwengu wa kuimba nyimbo za injili.Lakini baada ya dada yangu GRACE WAGANA akishirikiana na mama mchungaji wakawa wanaongoza ibada wanaimba,nami nikawa nazidi kutamani sana kuimba kama yeye.Kwa hiyo katika kutamani huko na mimi nikawa naimba,basi kuna mama yangu mmoja wa kiroho akanitabiria kuwa baada ya mwaka mmoja nitakuwa mwimbaji wa kimataifa kipindi hicho sikuwa na maono ya kuingia studio kurekodi,nikasema huyu mama nini tena mbona hata dalili sizioni?Lakini nilipokea lile neno nikaondoka nalo nimefanya kazi kwa muda mrefu kweli,hatimaye nikaingia studio kweli.Lakini wakati mwingine unakutana na majaribu hadi natamani siku niliyoenda studio kurekodi ingetokea hata nikwajikwaa nikarudi nyumbani! Kwa kweli majaribu ni mengi,unakutana na vitu vingi,unakatishwa tamaa,yaani kwa kweli inahitaji moyo.

IK:Tumezoea kwamba mtu anapoingia katika fani yoyote lazima kuna mtu ambaye alimvutia ambaye yuko katika ile fani.Kwa upande wako wewe nani aliyekuvutia hadi ukaamua kuwa mwimbaji wa nyimbo za injili?

NEEMA MBISE:Kwa kweli mimi aliyenivutia hadi nikatamani kuwa mwimbaji,hapana.Ila baadae baada ya kuingia katika ulimwengu wa muziki nilitokea kumpendaANN ANNIE,natamani kuimba kama yeye.Kuna vitu fulani anavyo natamani kuwa navyo.
Neema Mbise akiwa Studio akirekodi
IK:Ni changamoto gani unazokutana nazo katika kuutangaza ukuu wa Mungu kwa njia ya uimbaji?

NEEMA MBISE:Changamoto ni nyingi,kwa mfano unaweza ukaitwa mahali kwenda kuimba wiki nzima.Unaenda unahudhuria mkutano nauli labda ni ya kwako siku ya mwisho unamaliza mkutano mchungaji anajifanya kama vile hakujui kabisa na wala hana muda na wewe.Unajikuta ukilaumu ina maana katika kumwimbia Mungu hakuna faida yoyote? Changamoto ni nyingi tena kwa mimi kaka binti nakumbana na majaribu mengi sana.

IK:Ni malengo gani ambayo umeyaweka unapenda uyafikie wakati ukiwa katika uimbaji wa nyimbo za injili?

NEEMA MBISE:Malengo yangu natamani nifike mbali tena mbali sana,kwa maana sasa hivi niko chuo cha biblia baada ya miaka mitatu nitakuwa mchungaji kamili.Lakini 2010 nilikuwa mwimbaji lakini pia niliweza kuingia darasani na kusomea mambo ya uandishi wa habari.

IK:Vijana ni nguvu kazi ya taifa,lakini vijana hawa hawa leo wadumbukia katika matatizo mengi.Ukiwa kama kijana unawashauri nini vijana ambao wanajihusisha na utumiaji wa madawa ya kulevya hasa ambao wako katika mazingira hatarishi?

NEEMA MBISE:Kwa kweli mimi nawaombea tu kwa Mungu awaokoe.Kwani wapo amabao wamejiingiza huko bila kujua.Wakijitambua wanaweza kutoka.

IK:Najua kuna watu walifanikisha mafanikio yako hadi sasa,ambao wamefanya hadi mimi na wengine wengi wamtambue NEEMA MBISE ni nani...

NEEMA MBISE:Napenda kwanza kumshukuru Mungu kwa yeye ndio muweza wa yote ambaye amesababisha hata wewe uweze kunipigia simu na kufanya hili unalolifanya.Napenda kumshukuru dada yangu GRACE WAGANA ambaye ameweza kunifanya niokoke.Sisi katika familia yetu tumeokoka wawili tu,mimi na dada yangu ambaye ni Grace,wengine wote bado wako Lutheran.Napenda kumshukuru sana maana bila yeye sijui hata ningekuwa wapi.Pia namshukuru Mchungaji wangu Mwampusa,ambaye amekuwa akinipa support hadi Neema nimefika hapa.
Ann Annie (kushoto) akiwa na Neema Mbise
IK:Waimbaji wengi wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kutangaza nyimbo zao.Mbona wewe hujaweka wimbo hata mmoja youtube?

NEEMA MBISE:Hata mimi sijui ni kwa nini sijaweka,watu wengi wameisha niambia niweke nyimbo youtube,labda nimpe mtu anifanyie.Sina jibu sahihi kwa nini sijaweka.

IK:Ni neno gani la mwisho wakati tukielekea ukingoni mwa mahojiano yetu ungependa kuwaambia wasomaji na wapenzi wa nyimbo za injili kwa ujumla?

NEEMA MBISE:Mimi neno la mwisho napenda kuwashukuru watangazaji wote wa radio za mjini Moshi,Radio Safina Arusha,Radio Wapo,nawashukuru watangazaji wote ambao wananipa kampani Mungu awabariki sana,nawapenda na wazidi kuniombea...

IK:Basi kwa niaba ya crew nzima ya Injili Kwanza,tunakutakia mafanikio mema,masomo mema katika kujiandaa kuja kuwa mchungaji wa kondoo wa Bwana.Pia nikushukuru kwa kuchukua muda wako na kukubali wito wa kufanya mahojiano maalum na IK.

NEEMA MBISE:Nakushukuru na wewe pia kwa kutumia muda wako kunipigia simu ,kwa kweli nashukuru sana..

IK:Ameeeen!

NEEMA MBISE:Asante!

Kipengele: ,

KUHUSU NEEMA MBISE MINISTRY:
Ni Mchungaji na mwimbaji wa nyimbo za injili hapa Tanzania!

0 Maoni