UMUHIMU WA MAOMBI.

Unknown | 4:22:00 PM | 0 Maoni



Ndani yetu binadamu hakuna nguvu
zozote za kumshinda shetani.
Tunahitaji kukaa ndani ya Yesu ili
atupe uwezo wa kumshinda Shetani
(Rejea; Yoh 15:4-5). Pia Mungu
hawezi kutupatia nguvu za
kumshinda Shetani, au kitu chochote
kile bila ya kumwomba, maana hataki
kuingilia uhuru wetu wa kuchagua
tutakacho. Zaidi ya hayo, tunatakiwa
kumwomba atusaidie siku baada ya
siku, maana adui yetu hutuwinda
kila siku ili atuangushe. Katika Luka
18:1, Biblia inasema; “Imewapasa
kumwomba Mungu siku zote, wala
wasikate tamaa”. Hivyo Inatupasa
tufanye maombi ya binafsi, na ya
dhati kila siku ili tukue kiroho.

Kama tutatambua kuwa chanzo cha
nguvu zetu ni mbinguni, na kwamba
hatuwezi kujiokoa sisi wenyewe bila
msaada wa Mungu, basi hatutaacha
kuomba. Biblia inasema; “Ombeni
bila kukoma” (1The 5:17). Mungu
ametoa ahadi ya kutupatia
tuyaombayo kama tutayaomba
sawasawa na Mapenzi yake. Mathayo
7:7-8 inasema; “Ombeni, nanyi
mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona;
bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa
maana kila aombaye hupokea”. Cha
msingi cha kuzingatia hapa, ni
“KUOMBA KWA IMANI”, ukiamini ya
kuwa utaenda kupokea kile ambacho
umemuomba Mungu.
Mungu hujibu sala zetu zote.

Anaweza akatufanyia yale
tuyaombayo mara moja, au
akachelewesha kulingana na Mapenzi
yake. Lakini pia, Mungu ameahidi
kutusamehe dhambi zetu zote, kama
tukiziungama na kuziacha kabsa.
Biblia inasema; “Tukiziungama
dhambi zetu, Yeye ni Mwaminifu na
wa haki hata atuondolee dhambi
zetu, na kutusafisha na udhalimu
wote” (1Yoh 2:9). Hivyo Mungu
ametupa ahadi ya kutusamehe
dhambi zetu zote. Yesu
aliwafundisha Wanafunzi wake
kusali, na katika Sala hiyo, kuna
maneno yanayosema; “Utusamehe
dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi
tunamsamehe kila tumwiaye” (Lk
11:4).

Hivyo, masharti ya kusamehewa
dhambi zetu, ni “KUWASAMEHE
KWANZA WALIOTUKOSEA SISI”. Basi
kila mmoja wetu amwombe Mungu
ampe Moyo wa kuwasamehe na
kusahau wale waliomkosea, maana
bila ya kuwasamehe, Mungu hawezi
kutusamehe dhambi zetu sisi pia, na
tusiposamehewa, hatuwezi
kuokolewa.

Sisi tunaamini ya kuwa, hakuna
Maombi ya muhimu, kuliko maombi
ya kusamehewa dhambi, na
kuongozwa na Roho Mtakatifu. Kwa
maana, kama tukisamehewa dhambi
zetu, na kuongozwa na Roho
Mtakatifu, tunakuwa na nafasi kubwa
ya kuingia mbinguni, na kuuona
ufalme wa Mungu. Na hicho ndicho
kitu cha thamani kuliko vyote.
Hivyo, dumu katika Maombi kila siku
bila kukoma.

Kipengele: ,

KUHUSU NEEMA MBISE MINISTRY:
Ni Mchungaji na mwimbaji wa nyimbo za injili hapa Tanzania!

0 Maoni